Mahakama yatoa kibali cha kukamatwa Tundu Lisu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam imetoa amri ya kukamatwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu na kuamuru wadhamini wake kufika mahakamani hapo kujieleza kwanini
wasilipe fungu la dhamana kutokana na mshtakiwa huyo kushindwa kufika
kusikiliza kesi yake bila ruhusa.
Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio.
Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu,
Thomas Simba baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa
jana kutajwa lakini mshtakiwa wa nne Lissu hakuwepo mahakamani.
Hata hivyo, alijitokeza mdhamini wake
mmoja kati ya wawili Robart Katula kudai kuwa mshtakiwa huyo anaendesha
kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mwanza.
Hakimu alihoji kwa nini mshtakiwa amesafiri na kuacha kuhudhuria kesi yake bila kuomba kibali cha mahakama yake.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa mshtakiwa.
Hakimu Simba alikubali ombi la Jamhuri na
kutoa amri ya kukamatwa mshtakiwa na wito kwa wadhamini kufika
mahakamani Novemba 21, mwaka huu kujieleza kwa nini wasilipe fungu la
dhamana dhidi ya mshtakiwa kwa kushindwa kuhudhuria kesi yake.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni,
Wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa
magazeti, Ismail Mehboob.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati
ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu, Dar es Salaam, Lisu na wenzake
walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la
Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia Lissu na wenzake walidaiwa Januari
14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati
ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.
Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume
cha sheria na bila ya mamlaka waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa
Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana