Watu watatu wapoteza maisha kwa ajali ya gari wakati wakielekea katika harusi
Abiria
watatu kati ya tisa waliokuwa wakisafiria gari aina ya Toyota Noah
T.878 CZY wamefariki dunia baada ya gari hilo kuacha barabara na
kupinduka katika kona maarufu ya Mohammed Trans nje kidogo ya mji wa
Singida.
Ajali
hiyo ambayo pia imesababisha majeruhi watatu, abiria hao walikuwa
wakitokea Dar es Salaam wakielekea Tabora kwa ajili ya kushehekea harusi
ambayo ilipangwa kufanyika Ijumaa ya Oktoba, 29 kati ya Daniel Braisan
Marangu na Lightness Godwin wote wakazi wa Bunju jijini Dar es Salaam.
Kaimu
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Mayala Towo, alisema ajali hiyo
imetokea Oktoba, 27 majira ya saa mbili usiku katika kata ya Kindai
tarafa ya Mungumaji barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Aliwataja
abiria waliopoteza maisha yao kuwa ni Lucas Alle Killo (26) muhitimu wa
chuo kikuu Muhimbili na mkazi wa Boko,Tumaini Mwasongela (36)
mfanyabishara mkazi wa Boko na Lilian Samwel Msuya (48) mfanyabiashara
mkazi wa Mbezi,Dar es Salaam.
“Waliojeruhiwa
ni Josephine Beda (28) mkulima mkazi wa Boko Bunju, Mpeli Bukuku (25)
mkulima mkazi wa Kinondoni Mkwajuni na Anabela Jailos Sanga (32) mwalimu
mkazi wa Bunju, Dar. Wamelazwa hospitali ya mkoani mjini hapa na hali
zao zinaendelea vema,” alisema.
Kuhusu
ajali hiyo, Towo alisema Noah hiyo mali ya mchungaji wa kanisa la
Assemblies of God Basihaya Bunju, Dar, Michael Salaka, siku ya tukio
lilikuwa linaendeshwa na Gidion Kamungisha (50) mkazi wa Boko Bunju,
Dar.
Alisema
uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi
uliopelekea dereva Kamungisha kushindwa kulimudu gari hilo.
“Kwa
sasa tunamshikiria dereva Kamungisha kwa mahojiano na baada ya
uchunguzi kukamilika,tuatamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya uzembe na
kusababisha vifo,” alisema Kaimu kamanda huyo.
Alisema
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa
barabara kuwa waangalifu wawapo barabarani na kuendesha mwendo
unaokubalika katika eneo hatarishi na kuchukua tahadhari zote wakati wa
safari.
Eneo
hilo la kona ya Mohammed Trans, limebatizwa jina hilo baada ya basi la
kampuni hiyo ya jijini Mwanza kupinduka kwenye kona hiyo ya kuwaka moto
ulioteketeza zaidi ya abiria 20 ambao wamezikwa kwenye kaburi moja
kwenye eneo la kona hiyo.