SERIKALI MKOANI PWANI YAONGEZA MIEZI MITATU KUWABOMOLEA WALIO NDANI YA HIFADHI YA BARABARA NDANI YA MITA 60
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Bwawani Kibaha.
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist
Ndikilo akiingia kwenye uwanja wa Bwawani Mailmoja Kibaha kuzungumza na
wananchi kuhusiana na zoezi la bomoa bomoa lililosogezwa mbele hadi
January 23 mwakani.
Baadhi ya wananchi Mail moja Kibaha wakionekana kusikiliza mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo.
(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
SERIKALI mkoani Pwani ,imewaongezea
muda wafanyabiashara na wananchi waliojenga kwenye eneo la hifadhi ya
barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro waliotakiwa kubomolewa novemba
23 mwaka huu badala yake itakuwa January 2017.
Zoezi
hilo lilikuwa likihusisha walioingia ndani ya barabara hiyo kuanzia eneo
la Kiluvya-Tamco na soko la Mailmoja ambapo wameongezewa miezi mitatu
kutokana na soko jipya kuchelewa kujengwa chini ya halmashauri ya Kibaha
Mji.
Mkuu wa
mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,aliyasema hayo wakati alipokuwa
akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara hao na wananchi kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika viwanja vya Bwawani Kibaha.
Aliwataka wahusika hao kuanza kubomoa na kuhama kwa hiari ,ndani ya kipindi hicho kilichoongezwa kabla ya january 23 mwakani .
Hata
hivyo mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa wafanyabiashara hao hawataondolewa
hadi halmashauri ya Mji wa Kibaha itakapojenga soko jingine.
“Maandalizi ya kuhamia kwenye soko
jipya hayajakamilika na hakuna chochote kilichojengwa ambapo ni miezi
miwili imepita toka TANROADS walipotoa notisi kwa waliojenga kwenye
hifadhi hiyo kuondoka likiwemo na soko hilo”
“Maelekezo yametolewa na waziri wa
ujenzi ,uchukuzi na mawasiliano kwamba zoezi la bomoabomoa ni mita 60 na
siyo mita 120 kama ilivyoonyesha na kutangazwa na wakala wa barabara
Tanzania (TANROADS)mkoa wa Pwani,”alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi
Ndikilo alisema mkurugenzi Jeniffer Omolo kasema mkandarasi kapatikana
hivyo namtaka ajenge soko ndani ya siku 30 ili ibakie kujenga vizimba
na ujenzi uanze kuanzia wiki ijayo ili wafanyabiashara wapate eneo lao
la kufanyia biashara zao.
Alisema
ujenzi wa soko utafanyika kwenye eneo la Mnarani maarufu kama
Sagulasagula ama Loliondo na wanatarajia kutakuwa na huduma muhimu
ikiwemo maji na huduma nyingine zitapatikana.
Alifafanua
muda uliopangwa wa miezi mitatu sawa na siku 90 vitu vyote viwe
vimekamilika kwani hakutoongezwa muda mwingine hivyo wale waliojenga
kwenye eneo ambalo ni hifadhi ya barabara ndani ya mita 60 waanze
kuvunja wenyewe bila kusubiri kushurutishwa.
Mhandisi
Ndikilo anasema walionunua kwenye eneo la kitovu cha Mji wanapaswa
kujenga haraka.Huu ni wakati wa jamii kukubali mabadiliko hayo ambayo
yapo ndani ya sheria ili mji wa Kibaha uweze kuwa katika mpangilio
mzuri.
“Lengo letu ni halmashauri ya Mji
kuwa manispaa hivyo moja ya vigezo ni kupanga Mji huu ,wananchi
watuelewe na wote tunahitaji kupanga Mji wetu alisisitiza .
Nae mwenyekiti wa jumuiya ya
wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Pwani ,Abdallah Ndauka
alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kutoa muda huo ili kutekelezwa agizo hilo
na halmashauri.
Ndauka
alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa soko hilo umechukua muda mrefu
kutokana na baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo na kusababisha
mipango mingi kushindwa kukamilika.
Awali mkurugenzi wa mji wa Kibaha
Jeniffer Omolo , alikuwa na wakati mgumu baada ya wafanyabiashara kuinua
mabango wakitaka mkurugenzi huyo atumbuliwe ama mkuu wa mkoa wa Pwani
aondoke nae wakidai ameshindwa kuwajibika .
Kufuatia hali hiyo mhandisi Ndikilo ,alisema anatoa muda wa
miezi mitatu kuitisha mkutano mbele ya wananchi ambao watapiga kura
endapo kutakuwa na mtendaji ambae ni kero na ataondoka nae.
Alisema serikali
ya sasa si ya kubembelezana kwani inahitaji watumishi wa umma
wanaowatumikia wananchi badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha Jennifer alieleza kwamba mchoro wa soko ulizinduliwa tangu mwaka 2014 .
Alisema tatizo kubwa ni uhaba wa fedha licha ya mpango uliopo ni kumaliza ujenzi mapema iwezekanavyo.
Jennifer alisema soko kwa sasa litahamia eneo la Sagulasagula na fedha zipo na tangazo la kumpata mkandarasi limeshatoka.
Alisema endapo zoezi la bomoa bomoa
litafanyika itawasaidia halmashauri kupanga Mji na kuwa na kujenga
mabanda ya kupumzikia abiria eneo la stend ya sasa.
Kwa mujibu wa Tanroads mkoani
Pwani,awali zoezi hilo lilikuwa lifanyike mwezi agost lakini muda
uliongezwa hadi mwezi novemba na kudai wapo watu wengine walishawekewa
alama ya X tangu mwaka 2004 .
“Sheria
ya barabara ya mwaka 1932 na kufanyiwa marekebisho 1958 kifunga na 52
na marekebisho ya sheria ya barabara na 13 ya mwaka 2007 “
Taratibu
za sheria za usimamizi wa barabara kifunga na 30 (b) eneo la hifadhi ya
barabara,mita 120 sawa na futi 400 kwenda kila upande kutoka katikati
ya barabara ni marufuku kufanya maendelezo yoyote katika eneo hilo.