POLISI KUBISHA SHULE ZA MSINGI!

pob1
Askari Polisi kutoka kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Happy Mshana akiwaelezea wanafunzi wa shule ya Msingi Sombetini iliyopo jijini hapa aina za Ukatili dhidi ya Watoto huku wanafunzi hao wakionekana kumsikiliza kwa umakini. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
pob2
Mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Sombetini Jackson Mutalemwa akiuliza swali baada ya kupata elimu ya Ukatili dhidi ya watoto kutoka Ofisi ya Dawati la Jinsia na watoto mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
pob3
Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akisisitiza jambo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Sombetini wakati anatoa elimu juu ya Ukatili dhidi ya Watoto kushoto kwake ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Evelyn Simalenga. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
pob4
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Sombetini iliyopo jijini Arusha wakishangilia mara baada ya kupata elimu ya Ukatili dhidi ya Watoto iliyotolewa na kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto la mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
…………………………………………………………..

Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia kitengo chake cha Dawati la Jinsia na Watoto limeanza kutembelea shule za Msingi kwa nia ya kutoa elimu ya Ukatili dhidi ya watoto. Hayo yameelezwa na Mkuu wa kitengo hicho Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa anatoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Sombetini iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipokea malalamiko mbalimbali ya wanawake, wanaume na watoto wakiwa ofisini lakini wamegundua kwamba wanafunzi wengi wa shule za Msingi hawana uelewa juu ya vitendo vya Ukatili unaotokea miongoni mwao.
Akitoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao Mkuu huyo wa Dawati alisema kwamba baadhi ya watoto wanafanyiwa vitendo vya ukatili kwa kubakwa na kulawitiwa lakini ukaa kimya na wasijue nani wa kumwambia, hivyo kuwataka pindi wanapoona dalili za watu kutaka kuwafanyia vitendo vya aina hii watoe taarifa haraka kwa wazazi wao, majirani au walimu.
Alisema kumekuwa na mbinu tofauti tofauti zinazotumiwa na walaghai kama vile kumnunulia Mwanafunzi pipi, kumpa msaada wa kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani “lift”, kumpa pesa hali ambayo aliwaambia wanafunzi waikatae kwani sio watu wote wana nia nzuri na wao.
“Mara unapohisi kuna mtu ambaye anasogea karibu yako na kukudanganya kwa kukupa msaada wa lift au kukunulia pipi unatakiwa kutoa taarifa mapema kwa wazazi wako, walezi wako, majirani au walimu wako hali ambayo itasaidia kukuepusha kuingia kwenye matatizo”. Alisisitiza Mkuu huyo wa Dawati.
Alisema watoto wanaweza wakafanyiwa vitendo hivyo si kwa watu wa nje na nyumba zao tu bali hata watu wao wa karibu kwa maana ya wazazi au walezi wao wanaweza kuwafanyia vitendo hivyo, na kuwaeleza kwamba wana nafasi ya kuwaeleza majirani na walimu wao ambapo taarifa hizo baadae zitawafikia katika ofisi yao ya Dawati na wao kuchukua hatua mara moja.
Akizungumzia aina mbalimbali za ukatili askari wa kitengo hicho, Happy Mshana alisema kwamba ukatili upo wa aina tofauti tofauti kama vile ukatili wa kingono, ukatili wa kijinsia, ukatili wa Kisaikolojia, ukatili wa kielimu na kadhalika.
Alisema mara nyingi wanafunzi wanaathirika na ukatili wa kielimu ambapo hali hii inatokana na wazazi au walezi kuwazuia watoto wao kwenda shule huku wakiwa wanastahili kusoma, hivyo kuwataka pindi wanapoona wao au wenzao wanakumbwa na hali hii watoe taarifa kwa majirani na ikishindikana wawaeleze walimu wao.
Kutokana na elimu iliyotolewa na Dawati hilo iliweza kuibua hisia za wanafunzi mbalimbali ambao wengi waliuliza maswali ambayo yalijibiwa na askari wa kitengo hicho walioongozwa vyema na Mkuu wa kitengo hicho Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu, huku wengi wao wakionekana kushangilia baada ya mmoja wao kutaka adhabu ya kunyongwa itumike kwa watuhumiwa wanaokutwa na hatia kwa makosa ya ubakaji  na ulawiti badala ya kifungo.
Mwanafunzi wa darasa la sita aitwaye Jackson Mutalemwa ambaye pia ni Mwenyekiti  wa Klabu ya Haki za  Watoto (Children Right Club) alisema kwamba kitendo cha Dawati kutoa elimu shuleni hapo kimekuja muda muafaka kutokana na vitendo hivyo kuripotiwa kwenye Klabu yao mara kwa mara hasa wanavyofanyiwa watoto wa mitaani hivyo kuwataka wasiishie kwenye shule tu bali wawaelimishe pia watoto wa mitaani
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Evelyn Simalenga alisema kwamba Dawati la Jinsia na watoto limewafanya wanafunzi wake wawe na uelewa mpana zaidi hivyo utawafanya wawe makini na kushauri kwamba elimu hiyo iendelee kutolewa kwa wazazi ili wawe karibu na watoto wao.
Powered by Blogger.