MTENDAJI WA TEMESA AAGIZA WATUMISHI TEMESA DODOMA KUJIANDAA NA SERIKALI KUAHAMIA MAKAO MAKUU.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt Mussa
Mgwatu (kushoto) akizungumza na Meneja wa TEMESA Dodoma, Mhandisi
Bikulamchi (kulia) alipomtembelea ofisini kwake.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme TEMESA Dkt Mussa Mgwatu (mbele aliyekaa) akizungumza na
watumishi wa TEMESA Dodoma, katika ukumbi wa TEMESA Dodoma,
alipotembelea kituoni hapo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu(katikati) akiangalia kiwanja kwa
ajili ya ujenzi wa karakana mpya ya kisasa itakayojengwa Mkoani Dodoma
kushoto ni Msaidizi wa Meneja Bw. Hassan Sumbi na Kulia ni Meneja wa
TEMESA Dodoma Mhandisi Bikulamchi.
Picha zote na Theresia Mwami TEMESA Dodoma.
………………………………………………………………..
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amewataka watumishi kuanza kujiandaa
kwa kupokea kazi nyingi kwani hadi sasa Serikali na Taasisi zake tayari
zimeanza kuhamia Dodoma.
Alisema kuwa kuhamia Dodoma
kutaleta changamoto mbali mbali katika utoaji huduma za matengenezo ya
magari, umeme, elektroniki na viyoyozi kwani mahitaji ya wateja yatakuwa
ni mengi mno kuliko ilivyo sasa.
Dkt. Mgwatu alizungumza hayo
alipotembelea kituo cha TEMESA mkoani Dodoma kuona changamoto na
utendaji kazi na kuzungumza na watumishi wa kituo hicho.
“Tuanze kujiandaa kwa ajili ya
changamoto hizo, tusingoje kuulizwa kwanini hatukujiandaa wakati
tunafahamu kuwa serikali inahamia Dodoma na naomba mjipange kutoa huduma
ipasavyo” Alisema Dkt. Mgwatu.
Aidha Dkt. Mgwatu amemuagiza
Meneja wa TEMESA Dodoma Mhandisi Bikulamchi kuanza kuandaa utaratibu wa
namna ya kuendeleza kiwanja cha TEMESA Dodoma kilichopo eneo la Kizota
ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mahitaji ya mji wa Dodoma
yanayozidi kukua siku hadi siku.
“Ni mategemeo yangu kuwa katika
kiwanja hicho tutaweza kujenga karakana kubwa tena ya kisasa ambayo
itakuwa mfano mkoani hapa, ambayo itaweza kukidhi mahitaji yote ya soko
la mkoa huu na hata nje ya mkoa, sambamba na ujenzi wa ofisi mpya ya
TEMESA Makao Makuu” alisistiza Dkt Mgwatu.
Kwa mujibu wa Dkt. Mgwatu
karakana hiyo ya kisasa ikijengwa itakuwa na watumishi wa ufundi na
utawala kwa uwiano mzuri wenye kuzingatia taaluma husika ili kutoa
huduma zenye ubora wa hali ya juu. Aliongeza kuwa itatakiwa kufanyika
mabadiliko makubwa ili kuweza kuwapata watumishi watakaoweza kuendana
na kasi ya mabadiliko hayo katika kituo hicho.
Pia Dkt. Mgwatu aliwataka
watumishi wa TEMESA Dodoma kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma walizo
nazo, kuheshimu taaluma za wengine pamoja na kuzingatia maadili ya kazi,
kufanya kazi zenye ubora ili kuhakikisha wateja wanaridhika na kazi za
TEMESA na hivyo kuvutia wateja zaidi hata kutoka nje ya Taasisi za
Serikali.
Kwa upande wao wafanyakazi wa
TEMESA Dodoma wamemuahidi Dkt. Mgwatu kufanya kazi kwa bidii zaidi ili
kuongeza mapato ya kituo na kwa ubora wa kazi ingawa bado kuna
changamoto ya kupatikana vitendea kazi vya kisasa katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kila siku.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt.
Mussa Mgwatu yuko katika ziara ya kikazi kutembelea vituo vilivyopo
kanda ya Kati kuangalia utendaji kazi wake na kuona changamoto zilizopo
ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa maendeleo ya Wakala huo.