KIGOGO WA JESHI LA POLISI ASHUSHWA CHEO,MWINGINE ATUMBULIWA
Mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu
Jeshi la Polisi limemvua cheo mkuu wake wa kituo cha Himo (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Zuhura Suleiman kwa tuhuma za kukutwa na gari la wizi aina ya Toyota Rav4.
Pia, jeshi hilo limemfukuza kazi kwa fedheha (kwa kutolipwa haki zozote) ofisa wake mwingine wa cheo cha koplo, Federika Shirima ambaye naye anatuhumiwa kukutwa na magari mawili yaliyoibwa jijini Dar es Salaam.
Hatua ya jeshi hilo dhidi ya askari wake imekuja siku chache baada ya kufichuka kwa tuhuma hizo ambazo zilionekana kulipaka matope.
Alipohojiwa na wanahabari Jumatatu iliyopita kuhusu tuhuma za kukutwa na gari hilo lililoibwa pia Dar es Salaam, ASP Zuhura alikanusha na kusisitiza kuwa hazijui.
“Hiyo taarifa (ya gari) mbona siijui. Hakuna taarifa kama hizo,” alikanusha taarifa hizo ambazo baadaye zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa ambaye alikiri maofisa wake kukutwa na magari hayo, lakini akasema hawawezi kupewa adhabu kabla ya kuthibitika kuwa amefanya uhalifu.
“Makachero wetu wanashirikiana na kikosi kazi cha Dar es Salaam na watakapobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Taarifa zilizopatikana jana zilisema, ofisa mwenye cheo cha koplo alisomewa barua ya kufukuzwa kazi juzi jioni na muda huohuo na ASP Zuhura naye akasomewa barua ya uhamisho.
“Kwa cheo cha ASP mamlaka yake ya nidhamu ni katibu mkuu kwa hiyo kilichofanyika ni kumuondoa kwenye wadhifa wa OCS akisubiri uamuzi mwingine kutoka juu,” kilidokeza chanzo chetu.
ASP Zuhura alipotafutwa kwa simu jana ili kuzungumzia suala hilo hakupokea, lakini Koplo Federika alipopigiwa alipokea na kukana kufukuzwa kazi kisha kukata simu.
Kamanda Mutafungwa alipopigiwa simu alitaka atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na alipotumiwa na kuulizwa kuhusu suala hilo, hakukanusha wala kuthibitisha zaidi ya kujibu atafutwe leo saa 5:00 asubuhi.
Kukamatwa kwa maofisa hao kulitokana na kutajwa na mtandao wa wizi wa magari jijini Dar es Salaam uliokuwa mikononi mwa polisi, ambao walisafiri hadi Himo na kuyakamata.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema mtandao huo umekuwa ukipeleka magari ya wizi Arusha na Moshi.
Chanzo: Mwananchi