MGONJWA APASULIWA UBONGO KIMAKOSA, MKUU WA HOSPITALI APEWA LIKIZO YA LAZIMA.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya
Taifa ya Kenyatta nchini Kenya ametumwa kwenye likizo ya lazima baada ya
mgonjwa ambaye hakufaa kufanyiwa upasuaji wa ubongo kufanyiwa upasuaji
huo katika hospitali hiyo.
Hatua ya kumpa likizo Lilly Koros kwenye likizo ya lazima imetangazwa na
Waziri wa afya Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo inakusudiwa
"kupisha uchunguzi".
Kisa hicho ambacho kimewashangaza wengi kilitokea katika hospitali hiyo
wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu
ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.
Taarifa ya Bi Koros iliyotolewa Alhamisi ilisema maafisa wanne wa
matibabu walikuwa wamesimamishwa kazi, akiwemo msimamisi wa sajili ya
watu wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo.
Wengine ni mwuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, mwuguzi wa kuwapokea
wagonjwa kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji na afisa wa kuwatia ganzi
wagonjwa.
Bi Koros alisema kupitia taarifa kwamba kosa hilo lilitokea pale
mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.
Mmoja kati yao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.
Huyo mwingine alikuwa amefurwa kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.
Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji.
Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji
walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa
mgonjwa waliokuwa wanamfanyia upasuaji.
Bi Koros ameomba radhi na kusema "tunafurahi kuwatangazia umma kwamba
mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri kupata nafuu".
Wakenya walivyopokea habari hizo
Wakenya wameeleza hisia zao katika mitandao ya kijamii ya Twitter.
"Jinsi mambo yanavyoharibika kwa haraka Kenya National hospital"
"Ukienda na kitambi kwenye hospitali ya taifa ya Kenyatta, unaweza ukute unapelekwa wadi ya wajawazito"
Hili sio sakata la kwanza kukumba hospitali hiyo, mwezi wa kwanza mwaka
huu, waziri wa afya nchini Kenya Dkt Cleopha Mailu aliamrisha uchunguzi
ufanyike baada ya wanawake waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa
kingono.
Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao zilidai kina mama waliojifungua
wamekuwa wanashambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati wakienda kwenye
chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.
Tukio hilo liliibua maandamano na wanaharakati na wanawake walikasirishwa na usalama duni na utendaji kazi wa hospitali hiyo.
Kisa karibu sawa Tanzania
Kwa upande wa Tanzania, kisa kama hiki kiliwahi kutokea mwaka 2007.
Tarehe 8 Novemba, madaktari wawili wa upasuaji wa ubongo katika
hospitali ya rufaa ya Muhimbili walimpasua kichwa Emmanuel Didas kutoa
uvimbe ambao haukuwepo.
Wakati mgonjwa Emmanuel Mgaya, aliyekuwa na uvimbe huo alipasuliwa goti.
Madaktari hao walichukuliwa hatua na kufutwa kazi na mamlaka ya hospitali.
Makosa Uingereza na India
Si Afrika pekee ambapo makosa kama hayo hufanyika. Kipindi cha BBC cha
Victoria Derbyshire mwaka jana kilibaini kwamba makosa takriban 1,400
hufanyika kila wiki katika hospitali za kujifungulia kina mama nchini
England kila wiki.
Mwishoni mwa mwaka jana nchini India, mtoto aliyekuwa amedaiwa kufariki
baada ya kuzaliwa katika hospitali moja mji mkuu wa Delhi alibainika
kuwa hai jamaa zake walipokuwa wanaelekea kumzika.
Chanzo- BBC
Chanzo- BBC