WALIMU WATUPWA JELA MIAKA 40 KWA WIZI WA MITIHANI.

Na mwandishi wa makaliblog simiyu;
WALIMU wawili wa shule ya sekondari Nyawana na Shishani zilizopo Wilaya ya Bariadi na Itilima Mkoani simiyu wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja kwa kosa la kuiba na kuvujisha mtihani wa
Taifa wa Kidato cha nne.
Walimu hao waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu Issa Makene (40) wa sekondari ya Shishani pamoja na Solela
Mangura (26) mwalimu wa kujitolea shule ya sekondari Nyawa ambaye hakuwepo
mahakamani wakati hukumu ikitolewa kutokana na kuruka dhamana na kutokomea
kusikojulikana toka kutajwa kwa kesi mwaka 2013.
Awali akiwasomea shitaka linalowakabili walimu hao katika
kesi namba 176/2015, kabla ya hukumu kutolewa na Hakimu mkazi wa mahakama hiyo,mwendesha
mashitaka wa serikali Mosses Mafuru alisema tukio hilo lilitokea novemba 10,
mwaka 2013,katika shule ya sekondari Sagata.
Mafuru alieleza kuwa Mwalimu Makene akiwa Mkuu wa kituo cha
kufanyia Mtihani huo shule ya sekondari Sagata baada ya kupangiwa, siku ya
tukio wakati wa chakula cha jioni aliwalaghai askari waliokuwa wakilinda
mtihani katika kituo hicho.
Alisema kuwa Makene aliwaomba askari hao kumpatia ufunguo wa
chumba kilichokuwa kimehifadhi mitihani hiyo na baada ya kupatiwa alifungua
chumba na kwenda moja kwa moja kwenye kabati iliyokuwa imehifadhi mitihani.
Mafuru aliendelea kuelezea mahakama kuwa Mtuhumiwa mara
baada ya kufungua kabati hilo, alichukua bahasha ya mtihani wa somo la Fizikia
wa kuandika (paper one theory) kisha kwenda kuuficha chini ya uvungu wa kitanda
chake shuleni hapo.
Alieleza kuwa kesho yake baada ya mwalimu huyo kuchukua bahasha
hiyo novemba 11, 2013 Mtuhumiwa alichana bahasha kisha kutoa karatasi moja ya
mtihani huo na kumkabidhi Mwalimu mwenzake wa kujitolea Solela.
Alisema kuwa Walimu hao walikuwa kwenye harakati za
kuwapatia wanafunzi 15 wa shule hiyo ambao mwendesha mashtaka huyo aliwataja
majina yao kuwa ni Abasi Makwaya, Veronica Jonathan, Mboji Masike, Saka Masuki,
Milembe Mabula, Makula Saya, Prisca Jonathan.
Aliwataja wengine kuwa ni Getruda Senga, Buye Masike,
Msafiri Samson, Japhet Martine, Alex Jackson, pamoja na Khamis Nkwabi.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo Hakimu John Nkwabi aliwahukumu
washitakiwa hao kwenda Jela miaka 20 kila mmoja, kwa maelezo kuwa mahakama
imejiridhisha na ushahidi ulitolewa na upande wa mashtaka.
Akiongelea hukumu hiyo Afisa Elimu wa Mkoa Julias Nestory
alisema haki imetendeka na imekuwa fundisho kwa walimu wengine, huku akibainisha
kuwa hajafurahia kufungwa kwa walimu hao.
Aliwataka walimu hao kukata rufaa kama wanaona hawajatendewa
haki, huku akiwataka walimu wengine kuwa na nidhamu kazini kwa kufuata sheria
na kanuni za utumishi wa umma ikiwa pamoja na wanaopangiwa kusimamia mitihani kuachana
na vitendo hivyo.