WATU ZAIDI YA 3000 KUPATIWA HUDUMA YA MACHO SIMIYU.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akiongea na wananchi wa kata ya Ngulyati wilayani Bariadi waliofika kupata huduma ya kupimwa macho na kupewa miwani iliyokuwa ikitolewa na Taasisi ya Life Ministry.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akimvalisha miwani ya macho Bernadeta Katendele baada ya kupatiwa huduma ya kupimwa macho iliyokuwa ikitolewa na Taasisi ya Life Ministry katika kijiji cha Ngulyati 

WATU zaidi ya 3000 Mkoani Simiyu wanatarajiwa kufikiwa na huduma ya upimaji wa Macho na ugawaji wa miwani unaofanywa na Taasisi ya Life Ministry kwa kushirikiana na umoja wa madhehebu ya dini wilayani Bariadi mkoani humo.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkurugenzi wa Life Ministry Dismas Shekalaghe alisema wameamua kutoa huduma hiyo ya macho ili kusaidia jitihada za serikali katika kutatua changamoto ya macho inayowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali.

Shekalaghe alisema watatoa huduma hiyo katika kata ya Ngulyati, Dutwa na Luguru kutokana na maeneo hayo kuonekana kuathirika zaidi na tatizo uoni hafifi na mtoto wa jicho.
‘’Umoja wa madhehebu Bariadi wanatuelekeza maeneo yenye changamoto ya macho, watu wengi wamepoteza matumaini ya kuona...hawaoni mbali na wengine wana uoni hafifu, hivyo tunawapatia huduma na kupeleka upendo wa kristo’’ alisema Shekalaghe.
Aliongeza kuwa mwaka jana waliwafikia watu 500 na kutoa miwani kwa watu 300, lakini kwa mwaka huu watahudumia watu zaidi ya 3000 na kutoa miwani kwa watu 1500.

Shekalaghe alisema Taasisi hiyo inajikitika kutoa huduma ya afya kulingana na uhitaji, pia wanasaidia ujenzi wa zahanati ambapo kwa mwaka huu wamesaidia ujenzi wa zahanati ya Itubukilo yenye thamani ya shilingi milioni 85.

Aliongeza kuwa watu wazima macho yao yanaathirika na matumizi ya kuni, uoni hafifu kwa baadhi ya watu pia wengi wao wanakabiliwa na tatizo la mtoto wa jicho.

Bernadeta Katendele ni mmoja wa watu waliopatiwa huduma hiyo alisema kwa muda mrefu alikuwa ameathirika na vumbi la chaki kwa muda wa miaka 15, lakini baada ya kupata huduma hiyo na kupewa miwani ameanza kupata nafuu.

‘’Mimi ni mwalimu nimeathirika na vumbi la chaki kwa muda wa miaka 15, lakini baada ya kupatiwa huduma hii na kupewa miwani nimeanza kuona matokeo kwa sasa macho yangu hayaumi tena, nawapongeza life ministry’’ alisema mwalimu Katendele.

Awali akizindua zoezi la upimaji wa macho na kugawa miwani lililofanyika katika kata ya Ngulyati, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka alisema huduma hiyo imekuja wakati jamii ikiwa na uhitaji mkubwa wa huduma ya macho kutoka na hali ya maisha pamoja na matumizi ya nishati ya kuni ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo la uoni hafifu.

‘’Tunawapongeza Life Ministry kwa kuleta huduma hii, wakati watu wanaihitaji, tunawaomba umoja wa makanisa mkoa wa Simiyu tafuteni muda tukutane ili kujadili na serikali kwa sababu kuna mambo amzuri mnayafanya lakini mmekuwa mkisahaulika’’ alisema Mtaka.
Mtaka aliongeza kuwa jamii inatakiwa kusomesha vijana ili kupata madaktari wa macho wa baadae kuliko kutegemea madaktari wanaotoka nchi za nje.
MWISHO.
Powered by Blogger.