WANANCHI WAMKATAA MKUU WA WILAYA MBELE YA WAZIRI MKUU
WANANCHI
wa wilaya ya Kwimba wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na
mkuu wa wilaya hiyo Bw. Mtemi Msafiri baada ya kutoridhishwa na utendaji
wake.
Wametoa ombi hilo jana (Ijumaa, Februari 16, 2018) walipozuia msafara wa
Waziri Mkuu alipowasili katika Ofisi za Halmashauri ya wilaya Kwimba
zilizopo Ngudu kwa ajili ya kuzungumza na watumishi akiwa katika ziara
yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Wananchi hao walimkataa mkuu wao wa wilaya Bw. Msafiri kupitia ujumbe wa
mabango 17, ambapo Waziri Mkuu amewataka wananchi hao wawe watulivu
wakati Serikali inafanyia kazi malalamiko yao.
Wananchi hao wanadai kwamba Mkuu huyo wa Wilaya anatabia ya kuamrisha
polisi wawakamate kwa kisingizio cha uzururaji na kisha wanawekwa
mahabusu, ambapo baada ya muda wanatolewa na kwenda kulima kwenye shamba
lake.
Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kila mtumishi atambue majukumu
yake na ayatekeleze. “Hakuna atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza
nanyi mnatakiwa kutenda haki kwa kuwatumikia wananchi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mkuu huyo wa wilaya Bw. Msafiri,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba Bibi Pendo
Malebeja na wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli wanatekeleza
majukumu yao ipasavyo na kuwatumikia wananchi.
“Mkurugenzi katika kipindi chako chote cha utendaji kuanzia mwaka 2013
hadi leo, fedha nyingi za Serikali zilizoletwa Kwimba zimepotea na
hazijulikani zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika na muda wote
huo Halmashauri imekuwa inapata hati chafu.”
Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya
Kwimba wabadilishe mienendo yao na wawatumikie vizuri wananchi pamoja na
kuishi nao vizuri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, FEBRUARI 16, 2018.