Wachezaji Majimaji, makomandoo Njombe wazichapa kavukavu


MASAA mawili kabla ya pambano la ligi kuu ya Vodacom kati ya Njombe Mji na Majimaji FC kuanza kumetokea vurugu za hali ya juu zilizohusisha wachezaji na makomandoo wa Wanalizombe hao dhidi ya makomandoo wa Njombe Mji.
Chanzo cha vurugu hizo ni kile kilichoelezwa kuwa ni imani za kishirikina baada ya Majimaji kugoma kuingia uwanjani kupitia geti maalum lililoandaliwa kwa hofu ya kuhujumiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu mjini Njombe inaelezwa kuwa Majimaji waligomea geti namba moja na kutaka kutumia namba mbili ambalo walizuiliwa kabla ‘hawajajiongeza’ kwa kulazimisha kupitia kwenye uchochoro.
“Baada ya kuzuiliwa geti namba mbili walitumia mlango mdogo ambao si maalum ndipo wakakutana na makomandoo wa Njombe waliowazuia kabla hawajaanza kurusha mawe,” alisema.
Baada ya kuona mvua ya mawe ndipo wachezaji na makomandoo wa Majimaji walipoamua kujitetea kwa kuanza kupigana na wadau hao wa Njombe na kuzusha vurugu kubwa iliyodumu kwa dakika kadhaa kutokana na kukosekana kwa askari wa kutosha kutuliza vurugu hizo.
Katika tukio, beki Paul Maona amejeruhiwa vidole vya miguuni na hatoweza kucheza pambano la leo huku benchi la ufundi la Majimaji likithibitisha kuondolewa katika kikosi cha kwanza kwa beki huyo.
Powered by Blogger.