SERIKALI YAMKABA SHINGO DANGOTE
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko
ametoa siku 14 kwa uongozi wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoa wa
Mtwara kuingia mkataba na wachimbaji wadogo wa gypsum.
Biteko ametoa kauli hiyo leo Januari 21, 2018 baada ya kutembelea kiwanda hicho na kuzungumza na viongozi wake.
Amesema mikataba hiyo inapaswa kuwa na
kipengele cha kuwalipa ndani ya siku 30 baada ya kiwanda kukusanya
gypsum kutoka kwa wachimbaji hao, lengo likiwa ni kuleta ufanisi na tija
katika biashara zao.
“Nimekubaliana hapa kamishna wa kanda
atasimamia hili la mikataba kati ya kiwanda na wachimbaji wa gypsum.
Sehemu ya malipo itakuwa ndani ya mkataba na watalipa ndani ya siku 30,”
amesema.
Amesema wachimbaji hao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo yao baada ya kupeleka kiwandani bidhaa zao.
“Nimeambiwa wachimbaji hawa walikuwa
wanalipwa baada ya miezi mitatu lakini kwa mkataba huu ambao wataingia
na kiwanda sasa watakuwa wanalipwa ndani ya siku 30,” amesema Biteko.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
inalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo sambamba na wawekezaji ambao
wanapaswa kufanya kazi bila kusumbuliwa.
“Uwepo wa kiwanda hiki unawasaidia
wachimbaji wetu waweze kupata bei nzuri pamoja na kupata soko la uhakika
la kuuza bidhaa zao. Dangonte wameniahidi kwamba ndani ya muda mfupi
watatekeleza agizo hili,” amesema.
Biteko amesema lengo la ziara yake ni
kuwasaidia wachimbaji wa gypsum ambao hawana mikataba na kujikuta
wakibanwa katika uuzaji wa bidhaa zao.
Chanzo- Mwananchi