KIMENUKA MICHANGO SHULE YA KIPIKA
BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Matarawe
katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamekusanyika katika
eneo la viwanja vya Shule ya Msingi Kipika mjini Mbinga na kudai
warudishiwe michango yao ya fedha walizochangishwa kuanzia mwezi huu.
Wiki hii, Rais John Magufuli alitoa
tamko kupiga marufuku michango kwa shule za msingi na sekondari nchini,
akisisitiza kwamba yeyote anayekiuka agizo hilo anapaswa kuchukuliwa
hatua kali.
Juzi asubuhi, wakazi wa Mtaa wa Matarawe
ambao ni wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni Kipika, walikusanyika
baada ya diwani wa kata hiyo, Leonard Mshunju kuitisha mkutano wa
dharura ili kujua hatma ya michango ya fedha, mahindi na maharage
walivyochangishwa kwa chakula cha watoto wanaosoma shuleni hapo.
Baada ya ufunguzi wa mkutano huo, wazazi
hao walisema hawawezi kupingana na tamko lililotolewa na Rais Magufuli
kwani wakati wanachangishwa michango hiyo baadhi yao walikuwa wakipewa
vitisho huku wengine watoto wao wakikosa nafasi ya kuandikishwa kuanza
shule darasa la awali kutokana na kukosa mchango husika.
Naye Diwani wa Kata ya Matarawe, Mshunju
aliwataka wazazi hao watulie na kueleza kuwa lengo la mkutano huo ni
kutaka kufikia muafaka juu ya michango yao waliyochangishwa ya chakula
na fedha warudishiwe au la.
Pamoja na mambo mengine, baada ya
mvutano wa muda mrefu wazazi hao walifikia muafaka kwamba watarejeshewa
michango yao waliyochangia ifikapo kesho wakaichukue shuleni hapo.
Aidha, gazeti la Habarileo limebaini
pamoja na wazazi hao kuchangishwa michango, hapakuwa na risiti yoyote na
michango hiyo ilianza kukusanywa Novemba 30, 2017 na mwisho ilikuwa ni
Januari 8, mwaka huu.
Ukusanyaji wa michango hiyo ulikuwa
ukifanyika kwa mwaka mzima, watoto kuanzia darasa la awali walikuwa
wakichangia Sh 10,000 darasa la kwanza, la pili mpaka la saba Sh 5,000
pamoja na dumu mbili za mahindi na maharage.
IMEANDIKWA NA MUHIDINI AMRI - HABARILEO