ALLIANCE WASIMULIA NAMNA WALIVYONYONGWA NA KADI NYEKUNDU DHIDI YA DODOMA FC



 Baada ya Dodoma FC kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Alliance Schools katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Kundi C, kocha mkuu wa kikosi hicho, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, ameibuka na kusema kuwa, wapinzani wao hao wamevuna walichokipanda.

Juzi Jumamosi, Dodoma FC ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamuhuri, Dodoma, iliibuka na ushindi huo ambao Alliance wameulalamikia kwamba wapinzani wao wamebebwa baada ya kushuhudiwa wachezaji wao wanne wakitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu.

Julio amesema: “Unajua ukiingia uwanjani ukiweka akili ya kwamba utaonewa basi hata haki ikitendeka vipi utajiona umeonewa tu, hicho ndicho kilichowaponza Alliance na nawaambia kwamba wamevuna walichopanda. Wachezaji wao wamepata kadi nyekundu kwa uzembe wao na wala hatujabebwa.”

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Alliance, Jackson Luka Mwafulango, alisema: “Kiukweli kama soka letu limefikia hatua hii basi hatutafika mbali, nikwambie tu, mazingira ya kadi nne kwa wachezaji wetu yalipangwa na naamini kabisa Dodoma FC imeandaliwa kucheza ligi kuu msimu ujao.

“Nasema hivyo kwa sababu dakika ya 34 tukiwa bado hatujafungana, mchezaji wetu Geofrey Luseke aliruka juu na mchezaji wa Dodoma kuwania mpira, wote wakaanguka chini tena ndani ya eneo letu la hatari, cha kushangaza mwamuzi akamuita Luseke akampa kadi nyekundu ya moja kwa moja akaenda nje lakini hakusema iwe penalti.

“Dakika ya 43, Dickson Ambundo akatufungia bao la kwanza, dakika mbili mbele mchezaji wetu Wema Sodoki naye akatolewa uwanjani kwa kadi nyekundu, tukio lenyewe likiwa ni kupiga mpira kwa kichwa mwamuzi akasema alishika.

“Haikuishia hapo kwani dakika ya 65, nahodha wetu Hans Masoud akatolewa uwanjani kwa kadi nyekundu, mazingira ya hiyo kadi hakuna anayefahamu kwa sababu haieleweki. Kabla ya hapo, wao walisawazisha dakika ya 47.

"Dakika 90 matokeo yalikuwa 1-1, zikaongezwa dakika saba ambapo dakika tatu mbele Ambundo akatufungia tena bao la pili, tukawa tunaongoza 2-1.

“Mpaka zile dakika saba zinakamilika mwamuzi Andrew Shamba hakuwa amepuliza filimbi ya kumaliza mchezo, tukashangaa dakika ya 98 Dodoma wakisawazisha kwa bao la kupewa kabla ya kuongeza la tatu lililowapa ushindi dakika ya 104 ndipo mchezo ukamalizika.

"Lakini pia kwenye dakika hizo za nyongeza, mchezaji wetu mwingine Shaban Wilium naye alipewa kadi nyekundu na kukamilisha idadi ya wachezaji wanne waliopewa kadi hizo kwa upande wetu. Baada ya mechi, Julio akatuambia wametuchinja kwa kisu butu, kwa kweli inaumiza sana.”
Powered by Blogger.