TAMISEMI yatoa miezi 3 kwa wavamizi wa maeneo ya taasisi za serikali kuondoka

Kufuatia
kukithiri kwa uvamizi wa maeneo ya taasisi za kiserikali yakiwemo ya
shule za msingi na sekondari, vituo vya kutolea huduma za afya,
hospitali na masoko unaofanywa na baadhi ya watu kwa kujenga nyumba za
makazi na vyumba vya biashara.
Waziri
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George
Simbachawene, leo ametoa maagizo kwa Maafisa Ardhi na Wakurugenzi walio
chini ya mamlaka ya TAMISEMI kupima mipaka halisi ya maeneo ya taasisi
hizo pamoja na kuwaondoa watakao bainika kuyavamia maeneo hayo.
Simbachawene
ametoa muda wa miezi mitatu kwa maafisa ardhi hao, kukamilisha zoezi
hilo la upimaji, pia ametoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kusimamia zoezi hilo ili likamilike kwa wakati.
“Liko
tatizo kubwa la uvamizi wa maeneo ya kutolea huduma za kiserikali
ambapo watu wanafanya ujenzi wa nyumba na vyumba vya biasara kwa ajili
ya kujipatia kipato. Ziko shule ambazo maeneo yake yanakaribia kupotea,
bahati mbaya hayo maeneo wataalamu wa ardhi wana mamlaka nayo wenyewe na
hawayafanyii upimaji. Hali hii ikiendelea miaka ijayo utakuta maeneo
hayo yamekwisha,” amesema.
Simbachawene
ametoa maagizo kwa walioingilia mipaka ya maeneo ya taasisi za
serikali, kuondoka wenyewe kabla ya kuondolewa kwa nguvu.
“Wananchi
waliovamia maeneo ya taasisi hizo waondoke wenyewe vinginevyo hatua za
kuwaondoa kwa nguvu zitatumika.Mfano soko la Tandale karibu linapotea
kutokana na kuvamiwa na watu, natoa wito kwa jamii iliyozunguka maeneo
hayo kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali za mitaa wanapobaini kuna
uvamizi wa maeneo unatendeka,” amesema.
Aidha,
amepiga marufuku ujenzi wa vyumba vya biashara katika shule, masoko na
hospitali za serikali kwa vigezo kuwa ni vyanzo vya mapato kwa kuwa
vinaathiri muingiliano wa kiutendaji na utoaji huduma wa taasisi hizo.
“Ujenzi wowote uliopo na unaotarajia kufanywa uthitishwe kuanzia sasa,” amesema.