TAKUKURU YA MDAKA MGOMBEA AKIGAWA MLUNGULA



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Lindi imemkamata na kumshikilia aliyekuwa mgombea wa nafasi ya ukatibu wa kata wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), kwa tuhuma za kugawa fedha kwa ajili ya rushwa.
Akieleza tukio hilo, kamanda wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi, Stephen Chami alisema tukio hilo lilitokea jana katika kijiji na kata ya Kilangala, wilaya na mkoa wa Lindi, wakati wa uchaguzi wa marudio ndani ya chama katika kata ya Kilangala.

Kamanda Chami alimtaja aliyekamatwa na kushikiliwa na taasisi hiyo yenye dhamana ya kupambana na kuzuia rushwa kuwa ni Mohamed Njengu, aliyekuwa anashindania nafasi hiyo na Mohamed Nandala.

Chami alisema walipewa taarifa na viongozi wa CCM kwamba kuelekea siku ya uchaguzi kulikuwa na vitendo vilivyoashiria kuwepo rushwa kabla na wakati wa uchaguzi huo uliokuwa na wajumbe arobaini. Hivyo taasisi hiyo kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa mtuhumiwa huyo, wakala wake na waliogawiwa fedha ili kuwashawishi wamchague mgombea huyo.

“Tulipopewa taarifa tulikwenda kuweka mitego, siku ya uchaguzi tulimkamata wakala wake anayetambulika kwa jina la Mohamed Mbuta. Huyo bwana Mbuta tulimkuta na orodha ya majina, mengine yakiwa yamewekwa tiki kwamba wenye majina hayo walishalipwa shilingi elfu mbili kila mmoja,” alisema kamanda Chami.

Kamanda huyo alisema Mbuta alikiri kuwa alipewa shilingi 50,000 na Njengu awagawie wajumbe ili wanunue maji ya kunywa. Huku akibainisha kwamba Njengu ambae anashikiliwa na taasisi amekiri pia alimpa Mbuta kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuzigawa kwa wajumbe 34 waliorodheshwa kwenye orodha.

“Alichanga karata na kupiga hesabu vizuri za ushindi kupitia rushwa aliyokuwa anagawa kwa wajumbe. Alikuwa na uhakika wakupigiwa kura 34 kati ya 40 za wajumbe halali wa mkutano huo,” alibainisha Chami.

Chami aliwataja wajumbe waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo, ambao wapo nje kwa dhamana ni Mohamed Ñdongwele, Rashid Mkuwele, Seleman Chilu, Mohamed Tondolo na Mohamed Mpwatile.

Aliwataja wengine kuwa ni Elias Kawawa, Betrine Yakobo na Thobias Karatasi. Huku akibainisha kuwa takribani asilimia tisini ya waliopewa fedha wamekiri na wamerejesha fedha hizo.

Alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na maofisa wa taasisi hiyo. Ambapo baada ya kukamilisha uchunguzi kupitia mahojiano hayo atapelekwa mahakamani.

Mbali na hayo, kamanda Chami alitoa wito kwa wananchi kuwachagua wagombea kwa sifa ya uwezo wa kuwaongoza badala ya rushwa. 
Huku akibainisha kwamba kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, taasisi hiyo imejipanga vema kuhakikisha viongozi wagombea hawachaguliwi kwasababu ya uwezo wao wa fedha.

Kwa mujibu wa kamanda Chami uchaguzi huo wamarudio ulitokana na mtuhumiwa huyo kukata rufaa na kupinga matokeo ya uchaguzi wa awali. Ambayo yeye alishindwa kuchaguliwa kwa nafasi hiyo.

Powered by Blogger.