MWANDISHI WA HABARI ATEKWA,ATESWA KISHA KUPIGWA PICHA ZA UCHI ARUSHA.
Mwandishi wa habari wa kujitegemea
jijini Arusha, Lucas Muyovera amenusurika kuuawa kwa kipigo baada ya
kutekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Jumatatu Mei 14,2018.
Mwanahabari huyo ambaye kwa sasa
amelazwa katika hospitali ya Mkoa Mount Meru akipatiwa matibabu
inaelezwa hali yake ni mbaya baada ya watu hao wapatao watano kumteka
Jana majira ya saa tatu usiku katika eneo la Ngulelo jijini Arusha.
Kwa mujibu wa Mwandishi huyo watu
walimpakia kwenye gari yao na baadaye kumpeleka katika mto ambao
hajaufahamu na kuanza kumshambulia wakiwa wamemvua nguo zote na
kumdhalilisha.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Arusha Claude Gwandu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
"Ni kweli Mwandishi mwenzetu,Lucas
Myovela wa kituo cha Sunrise cha jijini hapa jana usiku
alitekwa,akapigwa sana,akapigwa picha za video akiwa uchi na kisha
akalazimishwa kutoa password ya simu yake wakampora pesa, Issue iko Polisi na watuhumiwa wamekamatwa,bado tunafuatilia kwa karibu",amesema Gwandu.
Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limethibitisha tukio hilo likidai bado wanafanya uchunguzi.