Wazazi watakiwa kuacha kuwatumia mabinti zao kama vyanzo vya mapato

Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias Tarimo, amewataka wazazi na walezi kuachana na dhana potofu ya mabinti zao kuwa ni vyanzo vya mapato kwa kuwaozesha mapema ili wapate mahari, watakao bainika kuendeleza vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesisitiza kwa kusema badala ya kukatisha ndoto za mabinti zao kwa tamaa ya mahari, badala yake wawekeze katika kuwasomesha, ili waweze kuja kumudu maisha yao na kuzinufaisha familia zao.
Tarimo aliyasema hayo wakati akizindua kampeni ya mradi wa ‘mapambao dhidi ya ndoa za utotoni ni jukumu letu sote’ katika wilaya ya Singida. Mradi huu unatekelezwa na shirika la World Vision Tanzania kwa ufadhili wa Watu wa Canada.
Akifafanua alisema kuozesha mapema binti ili mzazi/mlezi apate mahari ya mifugo au fedha taslimu, mali hizo kuwa hazidumu.
Akifafanua zaidi, mkuu huyo wa wilaya alisema binti akipewa nafasi na akafanikiwa kupata elimbora, uzoefu unaonesha kuwa wanazinufaisha familia zao kwa muda wote wa maisha yao.
“Hakuna hakuna jambo linamkera Rais wetu Dk. Magufuli kama mimba na ndoa za utotoni. Linamkera kwa sababu linakatisha watoto wa kike kuendelea na masomo yao. Serikali ya Rais Magufuli inatoa elimu bure ili watoto wa kike na wa kiume, wasome wawe na elimu bora, itakayo harakisha Tanzania kuwa na uchumi wa kati na ya viwanda,” alisema.
Mkuu huyo wa Wilaya, alisema mtoto yeyote aliye na umri chini ya miaka 18, kazi yake kubwa ni kusoma tu, na si vinginevyo.
“Mtoto wa kike au wa kiume kupata elimu ni moja ya haki yake. Kwa hiyo mtu ye yote anayeketisha mtoto wa kike kupata haki yake ya elimu, huyo ni mhalifu sawa sawa na wahalifu wengine. Hivyo anapaswa kuchukuliwa hatua ikiwemo ya kufikishwa mahakamani,” alisisitiza.

Awali mratibu wa World Vision Tanzania kanda ya kati, Faraja Kulanga, alisema kampeni hiyo iliyo zinduliwa, inatekeleza dunia kote na imeazishwa mwaka 2014.
Alisema kwa Tanzania, mkoa wa Shinyanga unaongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya ndoa za utotoni, na mkoa wa Singida ni wanane.
Alisema kwa ujmla kila mkazi wa mkoa wa Singida, anafahamu madhara ya ndoa na mimba za utotoni kwa watoto wa kike.
“Moja ya madhara hayo, ni kumkatisha masomo mtoto wa kike. Kauli ya kampeni hii ni ‘mapambano dhidi ya ndoa za utotoni ni jukumu letu sote’ , hivyo tunajukumu sote kuelimishwa jamii kitendo hicho ili waweze kuvichukia na kuviacha kabisa,” alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi wilaya ya Singida, Amina Abdallah, alishauri kuanzishwa kwa vituo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi wahanga wanaotokana na vitendo vya ndoa za utotoni na vingine ikiwemo ukeketaji.
“Watoto wengi hasa wa kike wanaoathirika na vitendo hivyo, hukimbia familia zao kitendo kinachochangia wakose makazi. Kwa hiyo, pakiwepo na vituo maalumitasaidia wahanga pamoja na mambo mengine, kuanza au kuendelea na masomo yao”. alisema Abdallah.