MTIBWA; MSITARAJIE KUTUFIKIA TENA.


Tangu msimu wa ligi kuu ya Vodacom 2017/18 uanze Agosti 26 kabla ya kusimama kupisha mechi za kimataifa na kuendelea tena wikiendi iliyopita, timu zote 16 zimecheza mechi mbili kila moja huku ushindani ukionekana kuwa mkubwa sana.

Hadi sasa Mtibwa Sugar inaongoza ligi ikiwa na pointi sita kufuatia kushinda mechi zote mbili. Mtibwa ilianza kwa kuifunga Stand United bao moja kabla ya jana kuifunga Mwadui FC kwa idadi hiyo hiyo katika uwanja wa Manungu.

Mtibwa ambayo inanolewa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Zuberi Katwila aliyechukua nafasi ya Mecky Mexime ambaye alitimkia Kagera Sugar msimu uliopita imekuwa ikifanya vizuri mwanzoni mwa ligi lakini ikifika katikati kasi yao inapungua na kujikuta ikiondolewa kwenye mbio za ubingwa.

Katika misimu kadhaa ya karibuni Mtibwa imekuwa ikishindwa kumaliza katika nafasi tatu za juu licha ya kuanza vizuri kama ilivyoanza msimu huu huku ikielezwa kuwa kuondokewa na nyota wao wa kikosi cha kwanza kila mwaka ndio sababu ya kikosi hicho kushindwa kuhimili vishindo hadi mwisho wa ligi.



Katika mahojiano , msemaji wa klabu hiyo Thobias Kifaru amesema kuwa msimu huu wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi na ikiwezekana kuchukua ubingwa kabisa akijiaminisha kuwa hawatoshuka tena kileleni.


“Tuna timu nzuri, tumekuwa tukiondokewa na nyota wetu kila mwaka lakini msimu huu tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri ikiwezekana tuchukue ubingwa,” alisema Kifaru.

Timu za Simba, Tanzania Prisons, Lipuli, Yanga na Azam FC zote zina pointi nne kila moja huku Singida United, Ndanda FC, Mbao FC, Mbeya City zikiwa na alama tatu.

Majimaji, Kagera Sugar na Ruvu Shooting zimefanikiwa kuambulia pointi moja kila moja wakati Stand United na Njombe Mji zikiwa hazijaambulia chochote mpaka sasa.
Powered by Blogger.