Kocha Big Bullets atua Mbeya City


KOCHA wa Big Bullets inayoshiriki ligi kuu nchini Malawi, Ramadhan Nsanzurwimo amemalizana na uongozi wa Mbeya City ili kuwanoa wagonga nyundo hao.

Raia huyo wa Burundi anakuja kuchukua mikoba iliyoachwa na mmalawi Kinnah Phiri ambaye mkataba wake ndani ya klabu hiyo ulivunjwa kwa makubaliano maalum baina ya pande zote mbili.

Siku nne zilizopita mtandao wa TIMES wa nchini Malawi uliripoti kuwa Nsanzurwimo amekuwa akidai malimbikizo ya mishahara yake klabuni hapo huku uongozi wa Bullets ukikiri kufahamu juu ya taarifa za kutua katika moja timu za hapa nchini.

Ramadhan Nsanzurwimo
Nsanzurwimo aliyewahi kushikilia jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Malawi anakabiliwa na jukumu la kurejesha kiwango cha City ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa haifanyi vizuri.

Kocha mzawa Maka Mwaluwisi alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kukalia kiti hicho lakini taarifa zilizotufikia ni kwamba jina lake liliondolewa dakika za mwisho kabla ya kukabidhiwa kwa mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Burundi.

Nsanzurwimo anakuwa kocha wa pili wa kigeni tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo inayomilikiwa na halmashauri ya jiji la Mbeya baada ya Phiri kudumu nayo kwa misimu miwili.
Powered by Blogger.