VILIO VYATAWALA MAZISHI YA KIJANA ALIYEUAWA KWA KICHAPO CHA WANAJESHI TANGA
VILIO, majonzi na simanzi vilitanda katika baadhi ya mitaa ya jijini 
Tanga ikiwemo Chumbageni na Nguvumali wakati msafara wa pikipiki na 
magari uliochukua mwili wa marehemu Salim Kassimu (18) mkazi wa Mwamboni
 jijini Tanga anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni
 askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mwili wa Salim ulikuwa ukitolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha 
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo ili kupelekwa nyumbani kwao 
eneo la Transfoma Mwamboni na baadaye kuhifadhiwa kwenye makazi yake ya 
milele baada ya kukabidhiwa kwa familia yake na kuzikwa jana asubuhi 
katika makaburi yaliyoko Masiwani Shamba.
Mjomba wa Marehemu, Abdi Shabani alisema walikabidhiwa mwili huo mara baada ya uc hunguzi wa Polisi kukamilika.
Baadhi ya wakazi walipozungumza katika mahojiano na mwandishi walisema 
marehemu huyo alikuwa akifanya kazi ya ukondakta wa daladala inayosafiri
 kati ya Nguvumali na Raskazone jijini hapa na inadaiwa alifia njiani 
wakati alipokuwa akipelekwa hospitali kupata matibabu baada kutekwa kwa 
saa kadhaa na kisha kupatiwa kipigo na baadaye kutekelezwa nje ya nyumba
 yao Mwamboni.
Huduma za daladala kutoka Kituo cha Nguvumali kuelekea maeneo ya 
katikati ya mji zililazimika kusitishwa kuanzia asubuhi kwa kile 
kinachodaiwa na madereva na makondakta kwamba ni kuomboleza msiba wa 
mwenzao huyo ambaye wanadai ameuawa kikatili.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuchukua mwili huo, Meya wa
 Jiji la Tanga, Mhina Mustafa Selebos aliwasihi wakazi hususan wa Kata 
ya Nguvumali kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa 
na mpendwa wao.
“Naomba wananchi tuwe wavumilivu wakati huu ambapo Jeshi la Polisi 
linaendelea na uchunguzi wa kifo cha huyu ndugu yetu... Kipekee 
nimpongeze sana Kamanda wa Polisi kwa ushirikiano alioutoa hadi 
kuwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa, nawaomba tuvute subira ili sheria 
iweze kufuatia, “alisema.
Naye mama mlezi wa marehemu, Salma Mnyamisi akizungumza mara baada ya 
mwili kufikishwa nyumbani alisema mwanaye amekufa kifo cha kinyama.
“Kwa kweli kifo cha mwanangu huyu ni cha kinyama naiomba serikali 
iingilie kati ili wahusika wa tukio la mauaji haya waweze kupatikana na 
kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Mwombolezaji Bwanaheri Athumani alisema amesikitishwa na tukio hilo la 
watu hao kujichukulia sheria mkononi na kuiomba serikali kuingilia kati 
ili kukomesha vitendo hivyo.
Naye Habibu Tunda alisema kumekuwepo na mwendelezo wa matukio ya uhasama
 na visasi baina ya raia na baadhi ya askari wa JWTZ wanaoishi katika 
kambi iliyopo Kata ya Nguvumali ambavyo mara kadhaa vimesababisha watu 
kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara kwa wakazi wa maeneo 
yanayozunguka kambi hiyo.
“Ili kukomesha ukatili huu tunaofanyiwa na hawa jirani zetu tunaomba 
Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wahusika wote bila kujali nyadhifa 
zao, “alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amethibitisha tukio
 hilo na kwamba watu watatu (majina yamehifadhiwa) wanashikiliwa na 
jeshi hilo kwa uchunguzi.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE-habarileo TANGA
 
 
 
 
 
 
