RAIS MAGUFULI KUWA MGENI RASMI SIKU YA SHERIA NCHINI
Rais
John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha
maadhimisho ya siku ya Sheria nchini zitakazofanyika mwanzoni mwa mwezi
ujao katika viwanja vya Mahakama jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na wanahabari jijini Dar es Salaam Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis
Juma amesema mahakama itawaelimisha wananchi jitihada mbalimbali
ilizochukua zenye lengo la kuboresha huduma zake kupitia mpango mkakati
wa miaka mitano inaoutekeleza katika kutoa haki kwa wakati na kuwezesha
ukuaji wa uchumi.
Amesema
kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, mahakama itafanya matembezi
maalum yatakayoongozwa na Rais Mstaafu Mh. Ali Hassan Mwinyi na
yataanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuishia katika viwanja vya
Mnazi mmoja.
Katika
matembezi hayo Mhe. Rais Mstaafu Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho ya
wiki ya elimu ya sheria ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuelekea
maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini.
Aidha
ametoa rai kwa wananchi kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili
ya utoaji elimu ya sheria nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata
huduma mbalimbali za Kisheria.
Alizitaja
huduma hizo ni pamoja na taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi
mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za mirathi, taratibu za kesi za
dhamana, taratibu za rufaa, ndoa na talaka, taratibu za kupokea na
kushughulikia malalamiko na Msaada wa Kisheria
Maadhimisho
ya Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka mwanzoni mwa mwezi wa
pili na mwaka huu yamebeba ujumbe wa Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati
Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.